• Breaking News

  Wizara yatenga Sh18.1 bil kujenga mahakama

  Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka 2017/18 imetenga Sh18.1 bilioni kwa ajili ya kujenga na kukarabati mahakama mbalimbali nchini.
   
  Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki alipokuwa akijibu swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi(CCM).
   
  Shangazi alihoji ni lini Serikali itakarabati majengo machakavu ya Mahakama ya Mwanzo Mtahe iliyopo kwenye Jimbo la Mlalo mkoani Tanga.
   
  Kairuki alisema azma ya Serikali ni kusogeza huduma za mahakama karibu na wananchi na kwamba katika mwaka wa fedha 2016/17 zilitengwa Sh 46.5 bilioni ambazo zimefanya kazi kubwa.
   
  Alisema mahakama ambazo zipo kwenye utaratibu wa kukarabatiwa ni Mahakama Kuu ya Tanga na Dar es salaam na kuanza ujenzi katika Mahakama Kuu ya Mara na Kigoma.
   
  Katika swali la msingi la Mbunge wa Njombe Mjini (CCM), Edward Mwalongo alitaka kujua kama Serikali itakuwa tayari kukarabati Mahakama za Mwanzo za Mahenye na Igomonyi ili wananchi waweze kupata huduma hiyo karibu.
   
  Akijibu swali hilo Kairuki alisema moja ya changamoto kubwa zinazoikabili Mahakama ni uchakavu wa miundombinu na ukosefu wa majengo ya kutosha.
   
  Alisema mpango uliopo ni kujenga majengo mapya na siyo kukarabati yaliyopo hasa ikizingatiwa kuwa majengo yaliyoombewa na mbunge yapo kwenye hifadhi za barabara na pia ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Njombe ni miongoni mwa miradi ya kipaumbele.
   
  Kuhusu Mahakama ya Mahenye alisema imeshapata nafasi katika Ofisi ya Kijiji cha Uwemba kwa ajili ya kuendesha shughuli za Mahakama ya Mwanzo Mahenye ili huduma iendelee kutolewa wakati mipango ya ujenzi inaendelea.

  No comments

  Post Top Ad