• Breaking News

  Bajeti Tano Za Wizara Zitakazopata Wakati Mgumu Bungeni

  Wakati Bunge likiendelea na vikao vyake mjini Dodoma, wizara tano zinatarajia kujikuta kwenye wakati mgumu mijadala ya hotuba zao za bajeti itakapowadia kutokana na matukio ya hivi karibuni.
  Wizara ambazo bajeti zake zinaweza kuibua mijadala mizito
  ni Wizara ya Elimu; Tamisemi; Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo; Mambo ya Ndani; na Wizara ya Nishati na Madini.
   
  Wizara ya Elimu inatarajiwa kukumbwa na mjadala kutokana na kutochukua hatua zozote tangu kuibuka kwa tuhuma za kughushi vyeti dhidi ya ofisa mmoja mteule wa Rais.
   
  Tangu tuhuma hizo zilipoibuka, si Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) wala Wizara ya Elimu iliyoibuka kuzungumzia suala hilo. Wizara hiyo inaendesha uhakiki wa vyeti vya elimu kwa watumishi wa umma.
   
  Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako, ambaye amekuwa akisisitiza uhakiki huo, amekuwa kimya katika suala la vyeti vya ofisa huyo.
   
  Mteule huyo wa Rais aliingia katika sakata hilo baada ya kuwatuhumu na kuwangaza wanasiasa, viongozi wa dini, wasanii na wafanyabiashara kuhusika katika matumizi na biashara ya dawa za kulevya.
   
  Tangu tuhuma hizo zitolewe dhidi yake, hajawahi kukiri wala kukanusha.
   
  Mjadala mwingine unaotarajiwa kuibukia wizara hiyo ni sera ya utoaji wa elimu bure. 
  Hivi karibuni Taasisi ya Haki Elimu imetoa taarifa inayoonyesha changamoto za utoaji wa elimu bure ikionyesha mafanikio hafifu.
   
  Mijadala itakayoibuka katika Wizara ya Elimu inaweza kufanana na mijadala itakayotokea Wizara ya Tamisemi inayosimamiwana George Simbachawene inayosimamia wakuu wa mikoa na wilaya.
   
  Hii inatokana na wakuu hao kuwaweka ndani watendaji kwa makosa ya kinidhamu kinyume cha Sheria ya Utumishi wa Umma inayoeleza bayana mamlaka za kuchukua hatua dhidi ya watendaji.
   
  Katika mijadala iliyoibuka awali, mbunge wa Muheza, Adadi Rajab alishauri wakuu wa mikoa na wilaya kuelimishwa kuhusu uchukuaji hatua na matumizi ya Sheria ya Tawala za Mikoa na Wilaya.
   
  Adadi aliyewahi kuwa kamishna wa polisi na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), alisema suala la ukamataji ni taaluma inayosomewa.
  Simbachawene pia ana kibarua cha kufafanua kuhusu changamoto za utoaji elimu bure.
   
  Hali kama hiyo inaweza kuibuka katika bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambayo kwa sasa inaongozwa na Dk Harrison Mwakyembe.
   
  Suala la waziri wa zamani, Nape Nnauye kutishiwa bastola na askari kanzu wakati akienda kuzungumza na waandishi wa habari linaweza kuibua mjadala wa uhuru wa habari na kujieleza.
   
  Dk Mwakyembe ana kibarua kigumu cha kufafanua kuhusu kukamatwa na kutekwa kwa wanamuziki, na hasa Ibrahim Mussa maarufu kama Roma Mkatoliki.
   
  Roma, akiwa na wasanii wenzake, walitekwa na watu wasiojulikana wakiwa katika studio ya Tongwe iliyopo Masaki jijini Dar es Salaam na baada ya siku mbili, walipatikana.
   
  Habari za watu waliowateka na mazingira ya kuachiwa huru zimekuwa na utata na hakuna aliyeweka bayana hadi sasa.
   
  Akichangia katika mjadala wa hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu wiki iliyopita, mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia alihoji sababu za Dk Mwakyembe kuhudhuria ambao Roma alikuwa anazungumza na waandishi wa habari kuhusu kutekwa kwake.
   
  Hoja ya Nkamia aliyewahi kuwa naibu waziri wa wizara hiyo katika awamu ya nne, ilikuja huku baadhi ya wabunge wakiibana Serikali iwajibike kwa matukio ya utekaji.
   
  Hata hivyo, Dk Mwakyembe alijibu hoja hiyo ya Nkamia kuwa alikuwa Maelezo kwa kuwa ndiyo ofisini kwake.
   
  Kabla ya tukio hilo la Roma, Elibariki Emmanuel, maarufu kwa jina la Ney wa Mitego, alikamatwa na Jeshi la Polisi baada ya kutoa wimbo wa “Wapo” unaoelezea kuwepo kwa watu tofauti, akiwemo kiongozi mwenye vyeti vya kughushi na kuhoji sababu za “mtumbua majibu” kutolitumbua “jipu jipya mjini”.
   
  Hata hivyo, Rais Magufuli aliagiza aachiliwe na auboreshe wimbo wake kwa kuongeza watu wenye sifa nyingine. 

  Katika muendelezo huo, matukio ya utekaji, ukamataji na mauaji dhidi ya viongozi wa vijiji, watendaji na askari wa Jeshi la Polisi, yanampa kibarua kigumu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba.
   
  Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete alimtaka Waziri Mwigulu kutoendelea kukalia kimya matukio ya utekaji, lakini siku chache baadaye polisi nane waliuawa katika shambulizi la aina yake lililotokea Kibiti mkoani Pwani.
   
  Pia, Waziri Mwigulu atakuwa na kazi nzito kutokana na kutotolea tamko vitendo vya utangazaji na ukamataji wa raia vilivyofanywa na mteule wa Rais kwa kuwalenga watu maarufu, wakiwamo wanasiasa, wafanyabiashara na wasanii walitajwa.
   
  Mbali na masuala ya usalama, hatua ya Rais Magufuli kukamata makontena ya mchanga wenye madini katika bandari ya Dar es Salaam, nalo linatarajiwa kuzua mjadala bungeni.
   
  Mbali na kukamata mchanga huo, Rais Magufuli amemsimamisha kazi katibu mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justine Ntalikwa saa chache baada ya kujibishana na ujumbe wa Spika Job Ndugai uliotembelea bandarini kushuhudia makontena yenye mchanga wa shaba.
   
  Suala hilo lilishaanza kuibua mjadala kutokana na hatua ya kuzuia ghafla mchanga huo, inayoonekana inaweka mazingira yasiyo rafiki kwa wawekezaji ambao walishangia mikataba na Serikali kwa kutumia sheria za nchi.
   
  Umoja wa wachimbaji wadogo uliiomba Serikali kuuachia mchanga huo kwa sababu unasafirishwa kwa kufuata utaratibu.
   
  Tayari Rais Magufuli ameshaunda kamati mbili za wataalamu kuchunguza mchanga huo na kutoa mapendekezo.
   
  Tangu mjadala wa mchanga huo uanze, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo hajatoa kauli yoyote

  No comments

  Post Top Ad